XtGem Forum catalog

Wananchi wanapewa bili za maji wasiyo tumia -Tulia



Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson ameitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kushughulikia tatizo la wananchi kupewa bili za maji huku maji hawapati kwa muda mrefu.

Naibu Spika ameyasema hayo katika kusisitiza swali la Mbunge wa Morogoro Mjini Abdul-Aziz Abood ambaye amesema Bungeni kwamba wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa muda wa miezi miwili wamekuwa hawapati maji lakini wanapelekewa bili ya maji na mamlaka ya maji ili kulipia bili hizo.

Akijibu Swali hilo Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Isack Kamwele amesema kwamba hii ni mara ya pili kupata malalamiko ya suala hilo hilo baada ya kupata kero hiyo alipokwenda Manispaa ya Mtwara Mjini.

''Kuna upotevu wa maji pamoja na wizi wa maji ndiyo unasababisha watu kupelekewa bili za maji ambazo hawajazitumia''- Amesema Naibu Waziri Kamwele.

Aidha Naibu Waziri amesema atawasiliana na mamlaka husika kuhakikisha wanatatua kero hiyo ili mtu alipe maji kulingana na matumizi.


RUDI