
Jeneza lenye mwili wa marehemu.
DAR ES SALAAM: Bado habari ni moto! Majonzi yanaendelea kutawala
kwenye familia ya Bilionea Erasto Msuya (43) aliyeuawa kwa kupigwa
risasi Agosti 8, 2013, Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia)
kufuatia safari hii, mdogo wake wa kike, Aneth Simon Msuya (30) naye
kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana, Uwazi limebaini
mchezo mzima.

Marehemu Aneth Simon Msuya
Aneth (pichani) alifanyiwa ukatili huo, Mei 26, mwaka huu chumbani,
nyumbani kwake, Block 16, Kibada- Kigamboni jijini Dar es Salaam akiwa
na mtoto wake, Allan Kimario.
Mauaji hayo yaligunduliwa na jirani asubuhi baada ya mtoto wa marehemu,
Allan kwenda kusema mama yake haamki na yeye anataka kwenda shule huku
basi la shule likiwa limemwacha. Pia alisema anahisi njaa.

Marehemu Erasto Msuya
Jirani huyo aliongozana na mtoto huyo hadi ndani na kuubaini mwili huo
ukiwa umalala sakafuni kwenye dimbwi la damu na kisu kilichotumika
kumchinjia kikiwa pembeni yake na hivyo kutoa taarifa polisi.

NI TUKIO LA KUSIKITISHA SANA
Tangu kutokea kwa tukio hilo, vyombo mbalimbali vya habari nchini
vimekuwa vikiripoti tukio hilo katika njia za kusikitisha sana kutokana
na unyama aliofanyiwa Aneth na ndipo, Uwazi nalo likazama mitaani
kuchimba kwa kina ili kuwapa wasomaji wake mambo mapya zaidi.

KUNA WATU WAMEPANGA KUIFUTA FAMILIA HIYO
Madai yaliyosambaa ni kwamba, kuna kundi la watu limepanga mkakati mzito
wa kuhakikisha familia ya Msuya inafutika kwenye uso wa dunia kutokana
na kisasi cha kibiashara (bila kufafanuliwa).
“Ilivyo ni kwamba, baada ya kaka yao (Erasto) kuuawa, kwa kupigwa
risasi, kuna kundi la watu limeamua kuifuta familia hiyo kwenye uso wa
dunia. Ndiyo maana mbali na Aneth kuchinjwa, kuna akina Msuya wengine
wameshakumbana na vitendo vya kuashiria kwamba, roho zao zinasakwa

HAUSIGELI ATAJWA MTUHUMIWA MKUU
Kwa mujibu wa chanzo kimoja toka ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania,
msichana anayedaiwa kufanya kazi za ndani ‘hausigeli’ nyumbani kwa
marehemu Aneth na kuondoka siku ya mauaji hayo, anapewa nafasi ya kwanza
katika kuchunguzwa akisemekena kuujua mchezo mzima wa kifo cha bosi
wake huyo na sasa jeshi hilo linamsaka kwa udi na uvumba.
“Kwanza nataka kusema kuwa, hausigeli ndiye mshukiwa wetu wa kwanza
ndani ya jeshi la polisi. Huyu msichana wa kazi aliondoka mchana, usiku
yakatokea yaliyotokea, akipigiwa simu hapatikani.
“Huyu tunamtuhumu kuujua mchezo wote. Kwa hiyo pa kuanzia kwetu
tunafanya juu chini kumpata ili aisaidie polisi,” kilisema chanzo hicho
huku kikiomba hifadhi ya jina kwa vile, si msemaji sahihi wa jeshi hilo.
ALIPANDIKIZWA?
Pia, chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, utafiti wa awali wa jeshi
hilo unataka kukubaliana kwamba, kutokana na mlolongo unaotokea wa
mauaji au kujeruhiwa kwa watu mbalimbali wa familia ya Msuya, kuna
uwezekano msichana huyo wa kazi alipandikizwa na watu hao kufanya kazi
kwa Aneth.
“Kuna wasiwasi yule dada wa kazi alipandikizwa. Kuna uwezekano alifika
pale katika njia za mtego ili kumsoma Aneth na mazingira yake pamoja na
mwenendo, sasa baada ya kukamilisha ndiyo akaamua kuondoka na usiku
wauaji wakafika. Kwa hiyo hayo yote sisi polisi tunayachunguza,”
kilisema chanzo.
WAUAJI WALIINGIAJE NDANI?
Kwa mujibu wa chanzo hicho, inaaminika kwamba, wauaji hao walifanikiwa
kuzipata funguo halisi za geti kubwa la mlango wa kuingilia sebuleni kwa
Aneth, wakaenda kuchongea nyingine ambazo siku walipofika, waliweza
kufungua geti na kuingia kama kwao.
“Lile geti kubwa linafunga kwa nje na funguo, kwa ndani unavuta loki tu.
Kwa hiyo wao waliingia ndani kwa kufungua. Walipomaliza kutenda ukatili
wao, inaonekana walifunga geti kubwa kwa kuloki ambapo kwa mtu mwingine
wa nje asingeweza kuingia ila yule mtoto (Allan) aliweza kutoka nje kwa
sababu loki yake ni ya kubetua tu.”
KWA NINI WAUAJI WALIIBA TIVII TU?
Chanzo hicho kikasema kuwa, watuhumiwa hao hawakuiba kitu zaidi ya tivii
(flat) lakini inaonekana kwamba waliamua kuichukua runinga hiyo kwa
vile waliamini ni skrini kwa ajili ya kamera za ulinzi (Closed-Circuit
Television au CCTV) ambapo walijua picha zao zilichukuliwa. Hata hivyo,
tivii hiyo waliitupa mbele ya safari.
HAIKUWA RAHISI KUMCHINJA ANETH
Chanzo hicho kilisema kuwa, mazingira ya chumba yalionesha kuwa, kabla
ya kuchinjwa, kulikuwa na purukushani kubwa kwani neti ilikutwa
imechanwa, baadhi ya vitu vimepinduliwa, vingine vimezagaa kila mahali
hali ambayo iliashiria kuwa, marehemu hakukubali kuchinjwa kirahisi.
MAISHA YA ANETH
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wakidai kumjua dada huyo,
walisema kuwa, baada ya kifo hicho wamebadili mawazo kuhusu yeye kuwa
huenda alijua anawindwa.
“Awali tulijua ni dada anayeringa, kwani alikuwa akifika dukani,
anaegesha gari jirani kabisa na mlango wa duka kisha anaagiza kitu
anachokitaka, anapelekewa, analipa pesa anaondoka.
“Hata siku tatu kabla ya kifo, alifika kwenye kibanda cha chipsi,
akaagiza na kufungiwa akiwa ndani ya gari. Alikuwa hana kawaida ya
kushuka, huenda alijua anawindwa,” alisema mkazi mmoja wa maeneo ya
Kibada huku akiomba hifadhi ya jina lake.
SIMU ZA KUULIZWA ALIPO
Mmoja wa watu waliodai kufanya kazi na marehemu wizara ya fedha, alisema
kuwa, wiki chache nyuma, Aneth aliwahi kusema kuwa, kuna wanaume
wamekuwa wakimpigia simu na kumuuliza; Aneth uko wapi?’ lakini akiuliza
we nani? Simu inakatwa!
“Huenda wale watu nao si sehemu ya watuhumiwa hawa. Maana hali hiyo
alisema hakuwahi kukumbana nayo siku za nyuma. Baada ya kusikia
amechinjwa sasa nahisi huenda Aneth alifuatiliwa kwa siku nyingi nyuma
lakini yeye alikuwa hajui,” mtu mmoja aliliambia Uwazi kwa kumkariri
mfanyakazi mmoja wa wizara hiyo.
MAISHA YAKE NA MAJIRANI
Baadhi ya majirani na nyumba ya marehemu walisema kuwa, haikuwa rahisi
kubaini mienendo ya watu wasioeleweka nyumbani kwa Aneth kwa vile maisha
yake yalikuwa hayasomeki kwa mwanga wa kawaida.
“Alikuwa akikuona anakusalimia akiwa ndani ya gari, akiingia kwake
ameingia. Sasa isingekuwa rahisi kumjua kwa undani yeye na wageni
wanaofika kwake. Lakini mimi nimewahi kusikia kwamba, Aneth aliolewa ila
kwa bahati mbaya ndoa yake ilivunjika mwaka mmoja na baba wa mtoto
wake,” alisema jirani mmoja kauli ambayo pia ilithibitishwa na dada
mmoja wa Aneth.
NDUGU WASHTUKA, WAWEKA MLINZI
Gazeti la Uwazi pia lilifanikiwa kufika nyumbani kwa marehemu ambapo
lilikuta nyumba inalindwa na mlinzi ambaye alisema aliwekwa hapo baada
ya mauaji hayo.
UWAZI OFISINI KWA RPC TEMEKE
Hayo yote yalikuwa maneno mbalimbali ya vyanzo vyetu, hivyo mwishoni mwa
wiki iliyopita, Uwazi lilifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Temeke, ACP Gilles Mroto ili kumsikia kama ana mtiririko huo, lakini kwa
upande wake, alisema kuwa, wapo katika msako mkali kuwasaka wauaji hao.
“Hata huyo hausigeli pia tunamsaka sana ili kulisaidia jeshi la polisi
kwa vile uondokaji wake na mauaji kuna utata,” alisema Kamanda Mroto.
MATUKIO YA KUIANDAMA FAMILIA
Tangu kutokea kwa mauaji ya Erasto, kumekuwa na matukio mengi ya kuiandama familia hiyo kwa kutaka kuwatoa roho wahusika.
KUNA ALIYEMWAGIWA SUMU
Dada wa Aneth aliyetajwa kwa jina la Antuja aliwahi kumwagiwa kitu
kinachosadikiwa kuwa ni sumu wakati akiwa amelala chumbani na mtoto wa
Aneth, Allan hivyo kuathirika na sumu hiyo.
TUKIO LA HONGERA BAR
Desemba mwaka jana, dada mwingine aitwaye Ester na muwewe walipigwa
risasi mgongoni na kifuani wakiwa katika Baa ya Hongera, Kijitonyama,
Dar.
Mwili wa Aneth alisafirishwa jana kwenda Kijiji cha Kairo, Mererani,
Simanjiro, Manyara kwa mazishi. Mungu aiweke pema peponi, roho yake.
Amina.